Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA AWAITA WACHINA KUWEKEZA VIWANDA VYA DAWA

Posted on: January 17th, 2026

Na WAF, Dar Es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini China kuwekeza Tanzania kwenye sekta ya viwanda vya Dawa na Vifaa tiba ikiwa na sehemu ya afua ya kuimarisha viwanda vya ndani ili kujitosheleza hadi kufikia asilimia zaidi ya 80 ifikapo 2030.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akihutubia jumuiya ya watu wa China kwenye sherehe za kuazimisha mwaka mpya wa nchi hiyo leo Januari 17, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania na China zimekuwa kwenye ushirikiano ndungu wa muda mrefu tangu enzi za baba wa taifa hayati Mwalimu Nyerere na Mao Sautong wa China.

Amesema udugu uliojengeka unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya pande zote mbili hivyo amewakaribisha kushiriki kwenye jukwaa la uwekezaji wa sekta ya dawa litakalofanyika Januari 19, 2026 jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano iwe inaweza kuzalisha dawa bila kutegemea dawa kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala Ubalozi wa China nchini Tanzania bwana Chen Hongchu amesema tukio la leo siyo tu la kusherehekea mwaka mpya, bali ni fursa ya kuimarisha urafiki na kuunganisha nguvu kwa pamoja.

Sherehe hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Watu wa mkoa wa Guangdong nchini Tanzania na Chama cha Urafiki kati ya Tanzania na China (TAN-CHINA Friendship Association)