Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATEMBELEENI WATOA HUDUMA ILI KUWAPA MORALI YA KAZI

Posted on: February 6th, 2025

Na WAF, Ikungi - Singida

Kaimu Mkurugenzi huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi huduma za Kinywa na Meno Dkt. Baraka Nzobo ametoa wito kwa wakurugenzi, wasimamizi na viongozi wa makundi mbalimbali kujenga utamaduni wa kuwatembelea watoa huduma katika vituo na maaeneo yao ya kazi hususani maeneo ya vijijini na pembezoni ili kuwaongezea morali ya ufanyaji kazi.

Dkt. Nzobo ametoa rai hiyo Februari 5, 2025 wakati wa zoezi la usimamizi shirikishi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Makiungu na Zahanati ya Dung’unyi wilayani Ikungi, mkoani Singida.

"Utekelezaji wa zoezi hili utasaidia watoa maamuzi kujua changamoto zilizopo maeneo ya kazi na vituoni hususani vijijini, nje ya miji na kwa watumishi na watoa huduma, jambo litakalosaidia kwenye uandaaji wa mipango ya bajeti na bajeti kwa ujumla kuwa na uhalisia" amesema Dkt. Nzoba na kuongeza.

“Ofisini tunakaa tunafanya kazi, lakini unapotoka kwenda kuwatembelea watoa huduma na watumishi kwenye vituo inaleta mwamko na ari ya ufanyaji kazi, lakini pia kuona hali halisi ya changamoto ambazo watumishi wanakutana nazo wakati wa utakelezaji wa majuku yao" amesisitiza Dkt. Nzobo.

Dkt. Nzobo amesema usimamizi shirikishi unasaidia kujengeana uwezo, kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma na kuboresha hali ya ubora wa huduma kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akitoa taarifa ya Hospitali Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Makiungu Dkt. Alesandro Nava imeainisha malengo ya hospitali hiyo ni kusogeza karibu huduma za afya za msingi na za kibingwa kwa watu wote na hasa watu wa mazingira ya kawaida na wa kipato cha chini, malengo ambayo hutekelezwa kwa kuandaa miundombinu ya afya, kutoa huduma bora za afya kwa gharama za chini, kipaumbele kikitolewa kwa huduma za mama na mtoto.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Dung’unyi iliyopo kijiji cha Munkinya wilaya ya Ikungi Bi. Advera Patrick amesema Zahanati inahudumia wananchi wapatao 13,191 kutoka vijiji vitano (5) vya Dung'unyi, Samaka, Damankia, Munkinya na Kipumbuiko.