Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATANZANIA WAHIMIZWA KUZIPA KIPAUMBELE HOSPITALI ZA NDANI KWA HUDUMA ZA VIPIMO

Posted on: July 10th, 2025

Na WAF - Dodoma


Watanzania wameaswa kuzipa kipaumbele hospitali za ndani ya nchi kwa kufanya uchunguzi wa afya wa awali kwa kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi katika Sekta ya Afya na zina uwezo wa kufanya uchunguzi huo hapa nchini. 


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Julai 10, 2025 alipofanya ziara katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) pamoja na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Jengo la 'Radio Therapy', Kuzindua Kliniki ya tiba utalii na kushuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya   BMH, JKCI na KCMC. 


"Tumezoea kufanya uchunguzi wa afya nje ya nchi tukiamini uchunguzi ukifanywa nje ndio unakuwa na majibu sahihi, kwa uwekezaji uliofanyika hapa Benjamini Mkapa, Muhimbili, MOI, Mloganzila na taasisi zetu nyingine  uwezo wa kufanya uchunguzi wa awali kwa sasa ni mkubwa na tunao," amesema Waziri Mhagama.


Aidha, Waziri Mhagama amesema  uanzishaji wa kliniki ya tiba utalii katika hospitali hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020, hivyo amewataka Wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi kuzingatia maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania na wageni wengi watakaokuja nchini. 


"Lakini wito wangu mwingine ni kwamba, vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwenye ngazi ya Kanda, Taasisi zinazotoa huduma za afya, Hospitali za Kanda, naomba tuanzishe huduma hii kama iliyoanzishwa na Hospitali ya Benjamini Mkapa kwa wale ambao hawana," amesema Waziri Mhagama. 


Amesema, Watanzania hawatakiwi kwenda nje ya nchi tena kwa kuwa Tanzania imeshaingia kwenye mfumo mzuri wa tiba utalii, huduma hizo zitaiwezesha Tanzania  kujitegemea yenyewe katika utoaji wa huduma bora na wageni kuja kwa wingi nchini kwa lengo la kupata huduma za matibabu. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Benjamini Mkapa Prof. Edward Hosea amesema kwa niaba ya bodi yake wamepokea maelekezo yote aliyoyatoa Mhe. Waziri Mhagama ikiwemo ya usimamizi wa M

mradi wa ujenzi wa jengo la Radio Therapy kukamilika hadi ifikapo mwezi Disemba 2025. 


Naye, Prof Abel Nkono Makubi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma za kibigwa 20 na kibobezi 17 ambapo pia inapokea wagonjwa zaidi ya 1,200 kwa siku. 


"Lakini pia katika hospitali yetu tunatoa huduma za upasuaji kwa njia ya matundu, kupandikiza uloto, upasuaji wa ubongo, mfumo wa mkojo pamoja na macho kwa kutumia tekinolojia ya kisasa," amesema Prof. Makubi.