Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WADAU WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA ENEO LA UPASUAJI WA UBONGO NA MISHIPA YA FAHAMU

Posted on: May 28th, 2024


Na WAF - Geneva, Uswisi

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Mei 28, 2024 amekutana kufanya mazungumzo na Prof. Gail Rosseau, ambaye ni bingwa wa upasuaji wa ubongo na mushipa ya fahamu kutoka Taasisi ya 'GW and Barrow Neurological Institute' ya nchini Marekani ambapo ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika eneo hilo.

Waziri Ummy amesema hayo leo Mei 28, 2024 wakati wa kikao chao cha pamoja na Prof. Gail Rosseau ambae pia ni Mwenyekiti wa Muungano uitwao 'G4 ALLIANCE (Global Surgery)' ambao ni muungano wa zaidi ya Taasisi 31 ambazo zinafanya kazi kwenye eneo la 'Neurosurgeon' katika nchi za Afrika.

Kupitia kikao hicho, wamejadili masuala mbambali ya ushirikiano katika eneo la upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu 'Neurosurgeon' ikiwemo kuwezesha mafunzo ya kibingwa kwa wataalam wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na kubadilishana ujuzi kwa kufanya mafunzo kazini.

Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau hawo kushirikiana katika kupata vifaa tiba (Implants) kwa bei nafuu kupitia muungano wa 'G4 ALLIANCE' wa nchini Marekani ili kuwezesha na kuboresha utoaji wa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu hususani katika Taasisi ya MOI.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu ameahidi kuanisha changamoto ambazo zitatekelezwa kwa ushirikiano na wadau hao katika kuboresha huduma za upasuaji wa ubongo.