Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WADAU SEKTA YA AFYA WAKABIDHI VITENDEA KAZI VYA THAMANI YA MILIONI 800 KWA SERIKALI

Posted on: February 23rd, 2024



Na. WAF - Tanga

Serikali kupitia Wizara ya Afya imepokea vitendea kazi vyenye thamani ya Milioni 800 kutoka kwa wadau wa CDC kupitia THPS kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI na Kifua Kikuu katika Mkoa wa Tanga.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amepokea vitendea kazi hivyo leo Februari 23, 2024 Mkoani Tanga ambavyo ni pikipiki 50, friji 72, Centrifuges 56, Compyuta 50, UPS 50 na printa 50 ambavyo vitendea kazi hivyo vitaimarisha huduma za Afya katika Mkoa huo.

Wakati akipokea vitendea kazi hivyo Waziri Ummy amewataka wote watakaokabidhiwa vifaa hivyo kuvitumia Kama ilivyo elekezwa ikiwa ni pamoja na kuwafikia wateja wanaoishi katika mazingira magumu na mbali na vituo vya kutolea huduma za Afya ili kuwafikishia huduma.

“Lakini pia tunaamini kwamba mtaongeza idadi ya huduma mkoba ‘outreach services’, kuwafikia wateja walio katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na kuwapatia huduma za kinga zikiwemo kinga dawa na kusafirisha sampuli kwa ajili ya kupima wingi wa Virusi vya UKIMWI.” Amesema Waziri Ummy.

Pia, amewataka kutunza vifaa hivyo na kuvifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kutimiza lengo la kudhibiti UKIMWI na VVU ambapo ametoa onyo kwa yeyote atakae fanya kinyume na maelekezo hayo kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Pia, Waziri Ummy Mwalimu ameyataka Mashirika yote ya kiraia yanayofanya kazi katika Sekta ya Afya angalau watenge kiasi kisichopungua asilimia 10 kwa ajili ya kuajiri watumishi wa Afya katika vituo vya kutoa huduma za Afya ngazi ya msingi.

“Tunaposema kupambana na masuala ya UKIMWI lakini kuna upungufu wa wauguzi, hakuna madaktari, hakuna watu wa maabara, hakuna wafamasia, angalau muajiri wauguzi wawili na watumishi wengine wa mikataba.” Amesema Waziri Ummy.