VIONGOZI WA DINI WAZINDUA JUMBE KUKABILIANA NA MALARIA NCHINI
Posted on: April 13th, 2024
Na WAF, ARUSHA
Viongozi wa dini nchini wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Alhaj Abubakar Zuber na rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wameongoza ujumbe wa viongozi wa dini kwenye zoezi la kuzindua jumbe za elimu kwa umma katika harakati zakutokomeza malaria nchini.
Hafla ya uzinduzi huo imefanyika Aprili 13,2024 jijini Arusha ambapo uzinduzi huo ni ishara ya kupeleka jumbe hizi sehemu mbali mbali ikiwepo kwenye nyumba za Ibada.
Akizungumza wakati wakati wa uzinduzi, Mufti Zuber amesema ibada zinategemea za waumini hivyo ni jukumu la viongozi wa dinu kuwaelimisha waumini wao umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa magonjwa ambayo vyanzo vyake vinaeleweka.
“Sote tunajua mazalia ya Mbu hutokana na maji na uchafu, tukiweka mazingira yetu safi, kwa namna moja au nyingine tutakuwa tumewasadia waumini kuepuka malaria na watahudhuria hata kwenye nyumba za ibada”. Amefafanua Mufti Zuber.
Kwa upande wake rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga amesema malaria ni ugonjwa unao wathiri watu wa rika zote na bila kujali hata itikadi zetu hivyo ni vema kuzingatia maelezo ya wataalam.
“Tumeambiwa kuna nchi zilishafuta Ugonjwa wa Malaria Zaidi ya Miaka 50 iliyopita, tusifikiri suala hilo lilikuja tu zilikuwepo jitihada za mtu mmoja mmoja, hivyo Mwongozo huu ambao tumeuzindua itakuwa vizuri kama utafikishwa hadi kwenye vigango na jumuiya zetu kuwaelimisha waamini” amesema Baba Askofu Nyaisonga.
Baba Askofu Nyaisonga, amewashauri watu ambao amekuwa wakikengeuka matumizi ya dawa na vifaa tiba kuacha hiyo tabia kwani miongoni mwa nchi 11 ambazo zinakabiliwa na Malaria na sisi tupo, tutumie mwongozo huu kama moja ya nyenzo ya elimu kwa umma.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mchungaji Lazoro Rohho aliyekuwa amemwakilisha Baba Askofu Fedrick Shoo, amesema wakristo lazima waache Imani potofu.
“Wapo baadhi ya wakristo, akiugua malaria badala yakwenda kuwaona wataalam wanakimbilia kwa watu ambao sio wataalam hali inayochangia wakati mwingine hata kupoteza maisha kwakuzani ni uchawi hii sio sawa” amesema Mch. Lazaro.
Akitoa salaam za Wizara, Mkuu wa Program Dkt. Catherin Joachim, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojiwekea mikakati yakutokomeza Malaria ifikapo 2030.
Mwongozo wa jumbe za kutokomeza ugonjwa wa Malaria, umezinduliwa na viongozi hao wa dini na umepangwa kusambazwa katika maeneo mbali mbali ya nyumba za ibada ili kuimarisha elimu yakuangamiza kabisa Malaria nchini
MWISHO