Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUWA MABALOZI KWA JAMII KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA.

Posted on: July 10th, 2025

Na. WAF, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa wito wa viongozi wa dini nchini kuwa mabalozi kwa jamii katika kutoa elimu ya namna bora ya kubadilisha mtindo wa maisha hususani kwenye lishe na kujenga taratibu za kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza. 


Hayo yamebainishwa Julai 10, 2025 Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowelle, wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa dini kuhusu elimu ya Kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.


Dkt. Gowelle amesema magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto kubwa, lakini pia  changamoto hiyo inaweza kushughulikiwa kupitia elimu, ushirikiano na mabadiliko ya mitindo ya maisha.


“Viongozi wa dini na wanajamii kwa ujumla mnalo jukumu muhimu la kusaidia kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya bora ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhali mapema ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na changamoto zinazosababisha afya ya akili,” amesema Dkt. Gowelle.


Ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, takriban asilimia 33 ya vifo vyote vinavyotokea nchini kila mwaka, husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza, ni sawa na mtu mmoja (1) kati ya  watatu (3) hufariki kutokana na maradhi hayo, jambo linaloathiri nguvu kazi ya taifa na kuongeza gharama za matibabu kwa familia na Serikali.


Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Tiba Dkt. Winfred Kilima amewataka viongozi wa dini na waandishi wa habari kutumia nguvu ya ushawishi waliyonayo kubadili mitazamo ya jamii na namna bora ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ili yasifike kwenye ngazi ya tiba.


“Tunatamani magonjwa haya yasifikie kwenye matibabu yaweze kuzuiwa na nyie viongozi wetu wa dini ni watu muhimu sana mnakutana na jamii ambayo ndiyo tunalenga elimu iwafikie kwa kiasi kikubwa,”amesema Dkt. Kilima.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Baraza la viongozi wa dini mbalimbali Tanzania, Askofu. Thomas Godda ameahidi kwa niaba ya dini zote nchini kutumia nyumba za ibada kwa ajili ya kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja  kubadili mtindo wa maisha yao, kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora na kuongeza kuwa ili binadamu aweze kufanya ibada anahitaji kuwa na afya bora.