Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UJUZI TULIOPATA KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA UTASAIDIA KUPUNGUZA RUFAA

Posted on: May 15th, 2024



Na WAF, Singida

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Dkt. Shaban Mahenge, amesema ujio wa madaktari bingwa wa Rais Samia utasaidia katika kupunguza rufaa za wagonjwa kutoka katika hospitali hiyo hatua ambayo inalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Singida na maeneo jirani.

Dkt. Shaban ameyasema hayo Leo, Mei 15, 2024 wakati wa kambi ya madaktari hao Pamoja na kupata mafunzo ya kibingwa juu ya kuwahudumia wananchi lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za kisasa kwa wananchi katika hatua za awali kabla ya rufaa.

“Uwepo wao umesaidia vituo vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida kupata ujuzi unaohitajika kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi”. Amesema Dkt. Mahenge

Aidha Dkt. Mahenge amesema kuwa anaamini kuwa ushirikiano kati ya wataalamu hao na watumishi wa afya wa ndani utasaidia kuimarisha mfumo wa afya na kutoa matibabu bora kwa wananchi.

Wananchi wa Singida na maeneo jirani wanatarajiwa kunufaika ujuzi, kwani utaboresha upatikanaji wa huduma za afya zenye viwango vya kibingwa na ubingwa bobezi katika eneo hilo.

Madaktari bingwa wa Rais Samia wameonyesha dhamira yao ya kuchangia katika kujenga mfumo imara wa afya nchini kote, na hatua ya kuanzisha huduma za X-Ray katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida ni sehemu ya utekelezaji wa azma hiyo.

Huduma za X-Ray zitawawezesha madaktari kufanya uchunguzi wa kina na kuweza kutoa diagnozi sahihi kwa wagonjwa, hivyo kuongeza ufanisi wa matibabu na kupunguza hitaji la rufaa kwa vituo vya juu vya matibabu.

Kwa kuongezea, mafunzo ya kibingwa yaliyotolewa kwa watumishi wa afya katika hatua za awali kabla ya kutoa rufaa yatasaidia kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma bora za afya kwa jamii. Hii ni hatua muhimu katika kujenga mfumo imara wa afya unaoweza kukabiliana na mahitaji ya wananchi kikamilifu.

MWISHO