UJENZI WA GHALA LA MSD DODOMA LAKAMILIKA KWA ASILIMIA 95
Posted on: February 6th, 2025
Na WAF, Dodoma
Ujenzi wa ghala la kuhifadhi bidhaa za afya la Bohari ya Dawa Kanda ya Dodoma lenye ukubwa wa mita za mraba 7,200, litakalogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 23.7 umefikia asilimia 95.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Februari 6, 2025 wakati akikagua ujenzi wa ghala hilo, Jijini Dodoma.
Amesema ghala hilo linatarajiwa kuzindiwa rasmi mwezi Aprili ambapo uzinduzi huo utaenda sambamba na uzinduzi wa ghala lengine mkoani Mtwara linalogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 18.
“Tunakwenda kuweka maghala mengine katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Songea, Chato, Iringa, Moshi na Arusha ikiwa ni muendelezo wa mikakati ya kuhakikisha mfumo mzima wa mlolongo wa usambazaji wa bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati, ubora unaotakiwa na kuhifadhiwa katika mazingira mazuri,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema kuwa Sekta ya Afya ina jukumu la kutoa huduma bora kwanza lakini ili kufanya hivyo inawapasa MSD kufanya biashara na kuzidi kuongeza mapato yake ili kuendesha shughuli zinazofanywa na bohari hiyo na kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Hatuwezi MSD kuendelea kuitegemea Serikali ni lazima tuiondolee mzigo serikali wakati huohuo tufanye mambo makubwa yatakayoifanya Serikali kutambulika kimataifa zaidi, kwa MSD kujitengenezea program mpya za kisasa zinazohusika kwenye ukanda wa Afrika na kujiuza ukanda wa SADC,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameitaka MSD kutopoteza muda baada ya mazungumzo na nchi za SADC, kuhakikisha wanaingia makubaliano kwa haraka na shughuli za kibiashara kwa mataifa yanaaza kwa haraka.
Waziri Mhagama amepongeza uongozi na watumishi wa MSD kwa kuendelea kuwa wabunifu kwa kufanya Tanzania kuwa kitivo cha usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwenye ukanda wa SADC na Afrika Mashariki na kupitia ghala hili ni uthibitisho kuwa itafikia kiwango cha juu cha kimataifa.