Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UFUATILIAJI, TATHIMINI NYENZO MUHIMU ZA UIMARISHAJI HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI

Posted on: September 26th, 2025

Na WAF - DODOMA

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kuboresha huduma za afya kuwa bora, thabiti na endelevu kwa wananchi wote kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Kutolea Huduma za Afya iliyo stahimilivu na endelevu (Resilient and Sustainable Systems for Health - RSSH) ili kuhakikisha utoaji wa huduma za afya zilizo bora na zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Akifungua kikao kazi cha kujadili rasimu ya mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya mradi huu utekelezaji wa mradi huu, Mratibu wa Dawati la Uimarishaji Mifumo ya Afya, Dkt. Hussein Juma Athumani amesema katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, wataalam wa afya wamekutana kupitia rasimu ya mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini katika kikao kinachofanyika katika Hoteli ya Royal Village, Dodoma, kuanzia Septemba 24 hadi 25, 2025,

Dkt. Hussein amesema Mradi wa RSSH unalenga kuimarisha mifumo ya afya kwa kuboresha huduma na kuongeza ustahimilivu wa sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali na wadau kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama.

“Tunataka kuhakikisha kuwa nyaraka hii inakuwa chombo sahihi cha kutuongoza katika kufuatilia utekelezaji wa shughuli za RSSH na kutathmini kama tunatimiza malengo ya kuimarisha huduma za afya stahimilivu na endelevu nchini,” amesema Dkt. Hussein.

Akizungumzia umuhimu wa zoezi hilo, Dkt. Hussein amesema ufuatiliaji na tathmini ndiyo nyenzo kuu ya kuhakikisha kuwa uwekezaji wa Serikali kwa kushirikiana na wadau, hususan Mfuko wa Dunia (Global Fund) unaleta tija kwa wananchi, na kuwasisitiza washiriki kushiriki kikamilifu katika kupitia na kuboresha rasmu hiyo, akibainisha kuwa kila mmoja ana nafasi muhimu kutokana na ujuzi na uzoefu alionao.

Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo matokeo mazuri ya ushirikiano wa Serikali na wadau wa maendeleo, Shirika la Maendeleo, Jumuiya ya Madola (Foreign, Common wealth and Development - FCDO) na Clinton Health Access Initiative (CHAI), ambapo jitihada zote zinalenga kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kote nchini.