Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UBUNIFU KATIKA SEKTA YA AFYA WAHITAJIKA KUBORESHA UFANISI KATIKA UTENDAJI

Posted on: September 26th, 2024

Na. WAF, Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, amewataka watumishi wa afya kuimarisha ubunifu katika utendaji wao ili kuendeleza ufanisi na kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika ziara yake leo Septemba 26, 2024, alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha, Bw. Rumatila amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma katika kuhakikisha kwamba sera ya afya inatekelezwa ipasavyo.

"ili kuendelea kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi na kufikia hadhi za juu zaidi ni vyema muwe wabunifu katika utendaji pamoja na kuzingatia miiko na maadili ya taaluma zenu, kufanya hivyo mtakua mmeitekeleza vyema sera ya afya ya kuboresha huduma za afya katika jamii". Amesema Bw. Rumatila

Aidha, ameipongeza Hospitali ya Mount Meru kwa kutoa huduma bora na za kiwango cha juu kwa wananchi, akisema kuwa hospitali hiyo inapaswa kuwa mfano wa kuigwa na vituo vingine vya afya nchini.

Pia, Naibu Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuongeza bidii katika kazi, akisema kuwa juhudi za watumishi wa afya ni muhimu kwa heshima ya Serikali kwani Kazi nzuri inaheshimisha Serikali na inatoa picha nzuri kwa wananchi.

Bw. Rumatila amesema kwamba uadilifu na uaminifu ni nyenzo muhimu si tu katika kutekeleza majukumu yao, bali pia katika kujenga imani miongoni mwa wananchi kuhusu mfumo wa afya kuongeza kuwa, vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa rasilimali, na ukosefu wa uwazi vinaweza kuharibu uhusiano kati ya watumishi wa afya na jamii, na hivyo kuathiri huduma zinazotolewa.

Mwisho Bw. Rumatila amewakumbusha umuhimu wa kuwasaidia wananchi wasiojiweza, akisisitiza kuwa ni muhimu kutowatenga wale walio na vigezo vya kutokuweza kumudu gharama za huduma za afya.