TANZANIA YAWEKA BAYANA UBUNIFU UNAOFANYIKA KUFIKIA AFYA KWA WOTE
Posted on: May 29th, 2024
Na WAF, Geneva Uswisi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeweka bayana mikakati na ubunifu unaofanyika kufikia malengo ya Afya kwa wote ifikapo 2030
Akizungumza wakati wa Mkutano wa pembezoni Mei 28,2024, jijini Genive Uswis, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kama nchi shabaha yao ni ifikapo 2030 lazima lengo hilo liwe limetimia.
“Kwa nchi za Afrika tukiongeza ubunifu unaofanywa na nchi zetu kwenye kuongeza wigo wa kutoa huduma za Afya na ugharimiaji malengo yetu yatatimia” amesema Mhe. Ummy
Waziri Ummy amefafanua kuwa maeneo ya ubunifu yaliyowasilishwa ni pamoja na Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Afya lililofanikisha kuanzishwa kwa Mfuko wa pamoja wa Afya ambao umewezesha kuimarika kwa utoaji huduma kwa ngazi ya msingi.
Ummy ameongeza kwamba eneo lingine ni ushirikiano na mashirika ya Kimataifa ni Global Fund, PEPFAR, USAID na CDC ambayo yameiwezesha Tanzania kuimarisha mifumo ya Afya ikiwemo kuongeza rasilimali fedha ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
“Kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi, Tanzania tumeweza kusogeza huduma za afya karibu na wananchi” amefafanua Waziri Ummy
Mjadala huo umefanyika pembezoni mwa kikao 77 cha Shirika la Afya Duniani kinachoendelea Geneva, Uswisi na kuwakilishwa Tanzania imewakilishwa
na Mhe Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe Nassor Mazrui (Mb), Waziri wa Afya, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar