Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAWEKA BAYANA MIAKAKATI KUPAMBANA NCDS

Posted on: February 7th, 2025

Na WAF, USWISI

Tanzania imeendelea kuimarisha mikakati yake ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kama sehemu ya juhudi za kuboresha afya ya wananchi.

Hayo yamebainishwa na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 156 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Ismail H. Rumatila, wakati wa wasilisho lake katika mkutano huo unaoendelea Geneva, Uswisi February 05, 2025.

Katika wasilisho hilo, Rumatila amesema Tanzania imeweka mfumo madhubuti wa kukabiliana na magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuanzisha mwongozo wa afya katika sera zote ili kuhakikisha uratibu mzuri wa jitihada za kinga na tiba.

Amesema nchi imeendelea kutekeleza mikakati mahsusi ya kuzuia na kutibu ugonjwa wa kisukari, afya ya kinywa na meno, pamoja na saratani.

Ameitaka WHO kuendelea kuziasa nchi wanachama kuhakikisha utekelezaji wa miongozo mbalimbali ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuzijengea uwezo ili kuzuia na kutibu magonjwa hayo, na kuimarisha mashirikiano ya kikanda kuweza kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

“Tanzania itaendelea kuimarisha mifumo yake ya afya ili kuhakikisha magonjwa Yasiyoambukiza yanadhibitiwa kwa ufanisi, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha afya bora kwa wote” amesema Rumatila.