TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA 80 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Posted on: September 25th, 2025
Na WAF – New York
Ujumbe wa Tanzania umeshiriki Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 80) unaofanyika New York Marekani, unaoongozwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, kuanzia Septemba 22 hadi 29, 2025.
Aidha, ujumbe wa Wizara ya Afya ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Ismail Rumatila, aliyeambatana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe pamoja na wataalamu mbalimbali, umeungana na ujumbe huo kushiriki katika mijadala na mikutano mbalimbali inayoendelea sambamba na Mkutano Mkuu.
Katika mkutano huo, Wizara ya Afya inashiriki majadiliano yanayohusu afua mbalimbali za kiafya kupitia Mjadala Mkuu (General Debate), mikutano ya pembezoni na mikutano ya uwili (bilateral meetings). Miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni pamoja na ajenda kuu ya magonjwa yasiyoambukiza.
Kupitia mikutano ya uwili, ujumbe wa Tanzania ukiwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie S. Kanza, umefanya mazungumzo na viongozi kutoka Ofisi ya Usalama wa Afya Duniani na Diplomasia tarehe 23 Septemba 2025 huku ujumbe wa Marekani ukiongozwa na Afisa Mkuu, Bw. Jeffrey Graham, akifuatana na Brad Smith (Mshauri Maalum), Rebecca Bunnell na Mamadi Yilla.
Mazungumzo hayo yamelenga namna Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika afua za kudhibiti VVU/UKIMWI, kifua kikuu, malaria, kuimarisha mifumo ya maabara pamoja na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko.