Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAPENDEKEZA KUNZISHWA KWA VITUO VIWILI VYA UMAHIRI KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI

Posted on: May 3rd, 2024



Na WAF - Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lipitishe maombi ya Tanzania kuanzisha vituo viwili vya umahiri kwa Afrika Mashariki vitakavyotoa huduma za Afya ya Kinywa na Meno pamoja na huduma za upandikizaji Uloto.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 3, 2024 kwenye Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Jijini Dar Es Salaam ambapo Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wamehudhuria.

“Chuo Kikuu cha Muhimbili kupitia idara ya kinywa na meno ina wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa, kwa hiyo tunataka wataalamu wote wa kinywa na meno wa Afrika Mashariki waje Tanzania kujifunza katika Taasisi yetu ya MUHAS.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema Tanzania inafanya vizuri katika masuala ya upandikizaji viungo ikiwemo upandikizaji wa Uloto hususan kwa watoto wenye changamoto za Sikoseli ambayo ni kati ya nchi Tano Duniani yenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na Sikoseli.

Aidha, Waziri Ummy amesema katika Mkutano huo wameweza kujadili kuhusu magonjwa Yakuambukiza ambapo kwa Bara la Afrika Mashariki inakabiliwa na changamoto za magonjwa ya Malaria, UKIMWI pamoja na Kifua Kikuu pamoja na magonjwa Yasiyoambukiza.

Amesema, ili kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza ni kuzingatia ulaji wa vyakula, kupuguza unywaji wa pombe na ufanyaji wa mazoezi, kwa Tanzania kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi imetengwa kuwa ni muda wa mazoezi ambapo Waziri Mkuu alitoa agizo la kufungwa na Daraja la Tanzanite kwa muda huo ili kuwapa uhuru watu wanaofanya mazoezi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Kenya Bi. Mary Muthoni amesema Jamii inapaswa kuelimisha juu ya Afya kwakuwa Afya inaanzia nyumbani, “usipokata vichaka shida inaanzia nyumbani, usipokula vizuri shida inaanza nyumbani, usipoweka maji safi na salama shida inaanzia nyumbani”.