TANZANIA YANUFAIKA KWA USHIRIKIANO NA CANADA
Posted on: April 24th, 2025
Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepata mafanikio makubwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na nchi ya Canada ikiwemo kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 67 hadi vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 kati ya mwaka 2016 hadi 2022.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 24, 2025 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwenye kikao cha pamoja na ujumbe kutoka nchini Canada ukiongozwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Emily Burns kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kuendelea kushirikiana katika Sekta ya Afya baina ya nchi hizo mbili.
"Pia tumefanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kutoka 43 hadi 33 kwa kila vizazi hai 1,000, vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 pamoja na kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameomba ushirikiano kutoka kwa nchi ya Canada katika kuimarisha mfumo wa wahudumu wa afya ngazi ya Jamii (CHWs), kuwezesha hatua za kutekeleza Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwa Wizara ya Afya inaendelea na utekelezaji wa mikakati hiyo.
"Serikali ya Tanzania imeajiri Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wapatao laki 137,000 ili kufikisha huduma muhimu za afya kwa jamii, lakini pia hatua ya kuanzisha Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ni katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa gharama nafuu na bila vikwazo vya kifedha," amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake, Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Emily Burns amemuahidi Mhe. Waziri kuwa Serikali ya Canada itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania kwa kutoa kipaumbele katika maeneo waliyoyaomba.
"Kwa kuwa Serikali zetu (Tanzania na Canada) zimekua na ushirikiano wa muda mrefu nami naahidi kuendeleza ushirikiano huo katika maeneo ambayo tutayapa kipaumbele ikiwemo eneo la wahudumu wa afya ngazi ya jamii," amesema Mhe. Balozi Emily.