Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA TAKWIMU SAHIHI ZA HUDUMA ZA AFYA YA MACHO

Posted on: September 23rd, 2025

NA WAF - MOROGORO

Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuna takwimu na taarifa sahihi juu ya huduma za afya ya macho nchini.

Hayo yamesemwa leo Septemba 23, 2025 mkoani Morogoro na Dkt. Best Magoma wakati akifunga kikao kazi cha waratibu wa macho wa mikoa nchini.

Dkt. Magoma amesema kuwa, pamoja na kuwa na miundombinu, vifaa na vifaa tiba, bado kuna umuhimu mkubwa wa kusimamia ubora wa huduma za afya ya macho ili kuhakikisha jamii inanufaika ipasavyo.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote wenye uhitaji, hususan maeneo yenye changamoto kubwa ya huduma hizo.

Dkt. Magoma amesema baadhi ya mikoa haina wadau au ina idadi ndogo ya wadau, jambo linalohitaji ushirikiano wa pamoja. Hatua hii inalenga kuhakikisha huduma hizo muhimu zinawafikia wananchi wote kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mratibu wa huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Greater Mande, amesema kuwa mikutano ya waratibu wa mikoa ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kuhakikisha huduma za macho zinatolewa kwa ufanisi.

Amehimiza ushirikiano kati ya mikoa ili kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi na taarifa za wagonjwa.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mikakati ya kitaifa unahitaji kila mkoa kutoa taarifa kwa wakati na kushirikiana na wadau wote. Hii itasaidia kuongeza ufahamu kwa jamii na kuboresha huduma za macho nchini.