SERIKALI YATEKELEZA MIKAKATI KUKABILIANA NA UDUMAVU NCHINI
Posted on: April 16th, 2025
Na WAF-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema inaendelea kutekeleza mikakati ya kupambana na tatizo la udumavu nchini kupitia Mpango kazi Jumuishi wa Lishe wa mwaka 2021/22 – 2025/26.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Nancy Hassan Nyalusi, leo Aprili 16, 2025 Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema, Serikali imeweka afua zenye lengo la kuboresha lishe kwa watoto na wanawake wajawazito.
“Baadhi ya afua zinazotekelezwa ni pamoja na kuhamasisha ulishaji sahihi wa watoto, ikiwemo unyonyeshaji wa maziwa ya mama, pamoja na utoaji wa elimu ya lishe katika vituo vya afya na kupitia vyombo vya habari,” amesema Dkt. Mollel.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inatoa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto chini ya miaka mitano, na kuimarisha uongezwaji wa virutubishi katika vyakula kama mafuta ya kula, unga wa ngano, unga wa mahindi na chumvi
kwa wanawake wajawazito,
Pia, Dkt. Mollel amesema Serikali inahakikisha mama mjamzito anapata vidonge vya madini chuma na asidi ya foliki wanapohudhuria kliniki ili kusaidia ukuaji bora wa mtoto tumboni na kupunguza hatari ya udumavu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi kwa wigo mpana zaidi na kutokomeza kabisa udumavu nchini.