Wizara Ya Afya

SERIKALI YAONGEZA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO KIGOMA

Posted on: August 19th, 2026

Na WAF - Kigoma

Wizara ya Afya, kupitia Idara ya Dharura na Maafa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea na zoezi la usimamizi shirikishi wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi, pamoja na kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika vituo teule vya afya mkoani Kigoma.

Zoezi hilo linalenga kutathmini na kuimarisha uwezo wa vituo hivyo katika kutoa huduma kwa wagonjwa na watu wanaoshukiwa kuwa na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola.

Timu ya wataalamu ikiwa Kigoma imeendelea kufanya ukaguzi na tathmini katika vituo teule, ikiwemo Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambayo ni miongoni mwa hospitali zilizotengwa kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa wa magonjwa ya milipuko. Ukaguzi huo pia unalenga kubaini mapungufu yaliyopo katika utoaji wa huduma, miundombinu, vifaa na utayari wa watumishi, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati na kuendelea kuimarisha uwezo wa hospitali kukabiliana na dharura za kiafya.

Akizungumza baada ya ukaguzi, Dkt. Erick Richard kutoka Wizara ya Afya amesema Serikali inalenga kuzuia magonjwa ya milipuko kuingia nchini na, endapo yatatokea, kuyadhibiti mapema ili yasienee.

Amesema Kigoma inaangaliwa kwa karibu kutokana na kuwa mkoa wa mpakani, huku Serikali ikiendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya ili wawe tayari kukabiliana na dharura za kiafya.

Kwa upande wake, Dkt. Umoja Erasto Chona, Mratibu wa Matibabu ya Magonjwa ya Mlipuko Mkoa wa Kigoma, amesema elimu kwa jamii inaendelea kutolewa kupitia viongozi wa dini, wazee maarufu na wanahabari, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuhakikisha taarifa zinatolewa mapema.

Naye Dkt. Samwel Roman, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, amesema hospitali hiyo iko tayari kutoa huduma za dharura, huku watumishi wakiwa wamepatiwa mafunzo na vifaa muhimu vya kukabiliana na Ebola na magonjwa mengine ya milipuko.

Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha utayari, mwitikio wa haraka na udhibiti wa magonjwa ya milipuko, hususan katika mikoa ya mipakani.