Wizara Ya Afya

AFRIKA ONGEZENI UWEKEZAJI WA AFYA YA MAMA NA MTOTO

Posted on: August 18th, 2026

Na John Mapepele

Tanzania imezitaka nchi zote za Afrika kuimarisha usalama wa afya na kujitegemea katika sekta ya afya kupitia uwekezaji endelevu na unaotabirika katika afya ya mama na mtoto, huduma za afya ya msingi, kuongeza fedha za ndani na uzalishaji wa bidhaa muhimu za afya nchini na kikanda.

Akizungumza katika Mkutano wa Nne wa Kamati ya Uongozi ya Mawaziri wa Afya ya Afrika Mashariki (ReSCO), unaofanyika jijini Dar es Salaam leo na kesho (18 -19 Agosti 2026), Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema Afrika inapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi la kuhakikisha inakidhi mahitaji yake ya afya.

"Afya ya mama na mtoto inapaswa kubaki kuwa kiini cha ajenda ya afya barani Afrika" huku akisisitiza kuwa vifo vya mama na watoto vinavyoweza kuzuilika ambapo kwa sasa bado viko katika kiwango kisichokubalika katika bara hili.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na maandalizi ya kukabiliana na milipuko katika mipaka ya nchi, wakati Afrika ikiendelea kukabiliwa na milipuko ya magonjwa, majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kibinadamu.

Mhe. Mchengerwa ameeleza mafanikio ya Tanzania katika kupanua upatikanaji wa huduma za afya ambapo amesema kati ya asilimia 80 na 85 ya Watanzania, sasa wanaweza kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka wanapoishi.

Pia vituo vya huduma za watoto wachanga vimeongezeka kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025. Vifo vya wanawake wakati wa ujauzito na kujifungua vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kati ya mwaka 2015 na 2022, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

Amesema, mafanikio hayo yametokana na kupanuliwa kwa huduma za afya ya msingi, kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya, kuboreshwa kwa huduma za rufaa za dharura kupitia mpango wa m-mama, kuongezeka kwa wataalamu wa afya wenye ujuzi, matumizi ya mifumo ya kidijitali, chanjo na kuimarishwa kwa programu za kudhibiti magonjwa