Wizara Ya Afya

TANZANIA YALENGA KUTOKOMEZA MALARIA IFIKAPO 2030

Posted on: August 18th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali imeendelea kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya malaria kwa kuimarisha afua za kinga, upimaji na matibabu, ikiwa na lengo la kutokomeza malaria nchini ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Agosti 18, 2026 Jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa niaba ya Waziri wa afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, ambapo amesema Serikali imeweka mikakati ya kupunguza maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Amesema watoto walio chini ya miaka mitano na wajawazito wanaendelea kuwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kuathirika na malaria, hivyo Serikali imeendelea kuyawekea kipaumbele katika afua za kinga na udhibiti wa ugonjwa huo.

Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutumia afua mbalimbali za kudhibiti mbu wanaoeneza malaria, ikiwemo matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu, upuliziaji wa viuatilifu ndani ya nyumba na viuadudu vya kibaiolojia katika kudhibiti mazalia ya mbu.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa tiba kinga ya malaria kwa wajawazito katika Halmashauri zote 184, huku watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 16 wakipewa tiba kinga katika Halmashauri zenye kiwango kikubwa cha maambukizi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Mhe.Dkt. Johannes Lukumay ameipongeza Wizara ya Afya kwa juhudi na azma ya kutaka kutokomeza malaria ambapo pia ameshauri kuongeza nguvu kupitia rasilimali watu na fedha ili kuongeza kasi ya kuunguza ugonjwa huo.

Aidha, amesema Kamati iko bega kwa bega na Serikali katika kuhakikisha huduma muhimu na afua za kutokomeza malaria zinafanikiwa ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa Waheshimiwa Wabunge katika utoaji wa huduma kwa jamii