WIZARA YA AFYA, CIHEB YAONGEZA UTAYARI WA KUKABILIANA NA EBOLA KAGERA
Posted on: August 21st, 2026Na Happyness Hans, WAF – Muleba
Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na CIHEB - Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola, kupitia usimamizi shirikishi wa huduma za dharura, ajali na wagonjwa mahututi katika Wilaya ya Muleba hususani hospitali ya Wilaya ya muleba na kituo cha afya cha kaigara mkoani Kagera.
Akizungumza leo Agosti 21, 2026, Mganga Mfawidhi wa Kitengo cha Dharura wa kituo cha afya cha kaigara, Dkt. Kulwa Kinyara, amesema wamefurahishwa na ujio wa timu ya wataalamu wa afya, akieleza kuwa ushirikiano huo ni fursa muhimu kwa watumishi kuongeza ujuzi na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, uangalizi maalum pamoja na huduma wakati wa milipuko ya magonjwa.
Dkt. Kinyara amesema ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na CIHEB umeendelea kuwajengea uwezo watendaji wa afya katika kuboresha huduma kwa wananchi, hususan katika maeneo yenye changamoto za magonjwa ya milipuko. Ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa mkoa wa Kagera kutokana na ukaribu wake na nchi jirani ambako magonjwa kama Ebola yamekuwa yakiripotiwa, hivyo kuongeza umuhimu wa kuwa na utayari wa kutosha.
Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Kitengo cha Dharura katika Kituo cha Afya Kaigara, Bi. Alidina Kokuilwa, amesema ujio wa timu hiyo umewapa fursa ya kupata elimu na uzoefu zaidi kuhusu utoaji wa huduma za dharura, udhibiti wa maambukizi na namna sahihi ya kuchukua hatua wanapokutana na wagonjwa wanaoweza kuwa na magonjwa ya milipuko.
Amesema mafunzo hayo yameongeza uwezo wa wataalamu wa afya katika kituo hicho na kuwafanya kuwa katika hali nzuri zaidi ya utayari wakati wa kutoa huduma, amesema kuongezeka kwa uwezo huo kutasaidia kuhakikisha wananchi wa Kagera, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya mpakani, wanapata huduma za afya zilizo salama, bora na kwa wakati.