Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAJIPANGA KWA MATIBABU YA SELI MUNDU KWA KUTUMIA CRISPR-CAS9

Posted on: February 8th, 2025

Na WAF, Dodoma

Serikali imesema kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya teknolojia ya CRISPR-Cas9, ambayo inatumiwa katika tiba ya ugonjwa wa seli mundu, na iko tayari kuanza kuitumia mara tu itakapothibitishwa rasmi duniani kote.

Akijibu swali la Mhe. Askofu Josephat Gwajima bungeni jijini Dodoma leo Februari 06, 2024, aliyeuliza Je, ni lini Serikali itaanza Matibabu ya Wagonjwa Wenye Selimundu kwa kutumia Crispr Gene Editing Technology?. Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa CRISPR-Cas9 ni teknolojia mpya ya uhariri wa vinasaba ambayo imeanza kutumika kwa binadamu kwa kipindi cha chini ya miaka miwili.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikifuatilia maendeleo ya tiba hii tangu mwaka 2022, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliifuatilia wakati wa ziara yake nchini Marekani.

“Mwaka 2024, suala hili lilikuwa miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika mikutano kati ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, na taasisi za tiba na teknolojia za Marekani. Wagonjwa waliotibiwa kwa teknolojia hii walihudhuria mikutano hiyo na kushuhudia maendeleo yake,” amesema Dkt. Mollel.

Kwa sasa, Naibu Waziri amesema kuwa tiba ya ugonjwa wa seli mundu inafanyika nchini kwa njia ya upandikizaji wa uloto (bone marrow transplant) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, huku Serikali ikiendelea kujiandaa kwa matumizi ya CRISPR-Cas9 mara tu itakapoidhinishwa rasmi kwa matumizi ya kimataifa.

Serikali imeanza matayarisho ya wataalam na teknolojia tangu mwaka 2022 ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kutumia tiba hii mpya na ya kisasa.