Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUWEKA KIPAUMBELE KWA MAMA NA MTOTO.

Posted on: April 14th, 2025

Na WAF, NJOMBE

Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa afya ya uzazi, mama na mtoto chini ya miaka mitano, hususan kwa lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na dharura za uzazi na watoto wachanga.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Juma Mfanga, ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wakati wa mkutano wa kanda wa tathmini ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, uliofanyika Aprili 14, 2025 mkoani Njombe na kukutanisha mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa.

Dkt. Mfanga amesema, Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kufanikisha azma hiyo, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya, kujenga vituo vipya, pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa watumishi wa sekta ya afya.

“Kupitia wataalamu mbalimbali wakiwemo mabingwa katika taaluma za afya, tumeendelea kutoa mafunzo kazini kwa lengo la kuwajengea uwezo watoa huduma, ili kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto na kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na dharura za uzazi na watoto wachanga eneo ambalo bado lina changamoto,” amesema Dkt. Mfanga.

Aidha, Dkt. Mfanga ameutaka mkutano huo kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza idadi ya wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji, pamoja na vifo vinavyotokana na njia hiyo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuzuilika kwa kutumia mbinu mbadala za kitaalamu.

“Tumekuwa na changamoto ya ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kupata matatizo yanayotokana na dawa za usingizi na ganzi, pamoja na hatari nyingine kama vile kutoka damu nyingi. Hili ni jukumu letu kuhakikisha tunachukua hatua za kulizuia,” ameongeza Dkt. Mfanga.

Awali, akitoa salamu za Wizara ya Afya, Mratibu wa Huduma za Watoto Wachanga na Watoto, Dkt. Angela Leonard, amesema lengo la mkutano huo ni kujadili na kutathmini utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, kubadilishana uzoefu, na kuweka mikakati bora ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kufikia lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika kanda na taifa kwa ujumla.