Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA HSE KUWAJENGEA UWEZO WATOA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: July 2nd, 2024Na WAF – DODOMA 


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Tasisi ya Health Service Executive (HSE)- Ireland zimepanga kushirikiana ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya.


Maafikiano hayo yamefikiwa leo Julai 02, 2024 wakati wa ugeni kutoka Ireland ukiongozwa na Prof. David Weaklim ambaye ni Mkurugenzi wa Global Health Service wa taasisi ya Health Service Executive (HSE)- Ireland ambayo inasimamia ubora wa huduma za afya nchini Ireland kwa kuambatana na Timu ya OR - TAMISEMI - Idara ya Afya.


Prof. David Weaklim ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na kuahidi kutoa ushirikiano kwenye eneo la kuboresha huduma za afya na kuongeza kuwa Mchakato wa kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Wizara umekamilika na utekelezaji utaanza hivi karibuni.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Wizara ya Afya Dr. Eliudi Eliakimu amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo na watalam wa afya kutoka ngazi za juu ili wawe na weledi wanapo kusimamia ubora wa huduma nchini hususani kipindi hiki cha utekelezaji Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance).


Nae Dkt. Pius Kagoma ambaye ni mratibu wa Uhakiki Ubora kutoka OR - TAMISEMI - Idara ya Afya, ameishukuru Timu ya Wataalam kutoka Ireland kwa kuwa tayari kutoa msaada wa kitaalamu na kuboresha huduma za afya kwa ngazi ya msingi (PHC).