Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI IMELENGA KUFIKIA 70% YA UCHANJAJI IFIKAPO DISEMBA 2022.

Posted on: July 6th, 2022

Na WAF - DOM 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kufikia asilimia 70% ya watu waliochanja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Dunia wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19. 

Waziri Ummy amebainisha hayo leo Julai 6, 2022 akiwa na Waziri wa TAMISEMI na Mwakilishi kutoka Wizara ya fedha katika Mkutano na Katibu Mkuu Msaidizi na Mratibu Mkuu wa Kimataifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka Umoja wa Mataifa Dkt. Ted Chaiban aliyeambatana na wajumbe kutoka WHO na UNICEF.

"Katika kikao hiki tumejadili kiundani mafanikio, changamoto na namna ya kuboresha Sekta ya Afya, na kama Serikali tumeridhia lengo la uchanjaji wa 70% ya watu wote Duniani ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya UVIKO-19." Amesema. 

Waziri Ummy ameendelea kusema kuwa, imetibitishwa kisayansi kwamba, ili kupata kinga kamili dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 inaelekezwa angalau 70% ya watu wote wawe wamepata chanjo ya chanjo hiyo.

Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema, Mpaka Julai 5, 2022 tayari watu milioni 8.5 wameshapatiwa Chanjo ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 na kuweka wazi kuwa, bado kuna kazi kubwa yakufanya ili kuweza kuchanja watu waliobaki ili kuweza kuishi na ugonjwa huo kama magonjwa mengine. 

Aidha, Waziri Ummy ameendelea kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kujitokeza kupata Chanjo ya UVIKO-19, hasa watu walio katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo kama vile wenye magonjwa sugu (Shinikizoladamu, kisukari, magonjwa, saratani, UKIMWI n.k) na wazee.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy ameendelea kusisitiza kuwa, Chanjo ya UVIKO-19 inatolewa kwa hiari, huku amewaelekeza Watoa huduma za Afya kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi ili kwa hiari wakapate chanjo ya UVIKO-19. 

Waziri Ummy, ameendelea kwa kupiga marufuku tabia za Watoa huduma kulazimisha wananchi wanaoenda kupata huduma kuchanja kwa lazima, na kusema kuwa tabia hiyo ni kinyume cha miongozo na maadili ya taaluma za Watoa huduma. 

Kwa upande wake, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa amesisitiza kuwa,  TAMISEMI itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya katika  kusimamia uboreshaji wa huduma za afya nchini.

Aidha, Waziri Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe .Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuifungua nchi na kukuza ushirikiano unaosaidia katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa UVIKO-19. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Msaidizi na Mratibu Mkuu wa Kimataifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka Umoja wa Mataifa Dkt. Ted Chaiban amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mfano kwa vitendo katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kupata Chanjo dhidi ya ugonjwa huo. 

Pia, ametoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kuendelea na kasi ya kutoa Elimu na uhamasishaji kwa wananchi ili wakubali kupata chanjo hiyo, huku akitoa pongezi kwa jitihada za kuongeza idadi ya waliochanja kwa muda mfupi kutoka asilimia 6.3 hadi kufikia asilimia 12.4. 


Mwisho