RUVUMA YAPOKEA MADAKTARI BINGWA 56 WA RAIS SAMIA
Posted on: October 28th, 2024
Na WAF - RUVUMA
Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapatao 56 wamepokelewa mkoani Ruvuma na uongozi wa mkoa huo kwa ajili ya kambi ya matibabu ya siku sita (6) katika wilaya zote nane (8) za mkoa huo, huku wakitakiwa kutoa huduma hizo kwa ufanisi mkubwa.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 28, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Ahmed Abas Ahmed wakati wa zoezi la kuwapokea madaktari hao katika viwanja wa ofisi ya Mkuu wa mkoa.
"Sina shaka na wataalamu hawa kwani najua wataifanya kazi hii kwa ufanisi, hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye vifaa tiba," amesema Kanali Ahmed.
Kanali Ahmed ametoa wito kwa viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi tarafa kuwapa ushirikiano wa kutosha madaktari bingwa na kuwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo adhimu kuchunguza afya zao na kupata matibabu ya kibingwa.
“Niendelee kutoa wito waheshimiwa wabunge na madiwani kuhamasisha jamii au wananchi kufika hospitalini kupata huduma stahiki,” amesema Kanali Ahmed.
Aidha Kanali Ahmed amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nanma anavyoipigania sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa kwa ngazi zote za Afya.
“Huduma hii ni muhimu kwa wananchi wetu, hasa katika vituo vinavyotoa huduma kwenye ngazi ya msingi, ni matarajio yangu uwepo wa kambi hii utatoa nafasi kwa wananchi kupata huduma stahiki kwakuwa kila hospitali ya wilaya itapokea seti ya madaktari bingwa wenye uwiano ulio sawa,” amesema Kanali Ahmed
Akitoa Salamu za Wizara, Afisa wa Idara ya Afya ya uzazi mama na Mtoto Bi. Grace Maliki, amesema zoezi hilo ni muendelezo wa zoezi la awamu ya kwanza baada ya kuwa na muitikio chanya.
“Hii ni awamu ya pili ya kambi ya Madaktari bingwa wa Rais Samia, ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 6 Mei, 2024 na kwenda katika wilaya zote 184 huku kukiwa na mafanikio makubwa, kwa mkoa wa Ruvuma kambi iliyopita iliweza kuhudumia wananchi zaidi ya 10,000 na kuwajengea uwezo zaidi ya wahudumu 334,” amesema Bi. Maliki.