Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MSD YAENDELEA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA DAWA, VIFAA, VIFAA TIBA HOSPITALI ZA RUFAA NCHINI.

Posted on: September 22nd, 2024

Na WAF – Mbeya

Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuimarisha ushirikiano na hospitali za rufaa nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati ili kuboresha huduma za afya kwa kurahisisha ugavi wa bidhaa za Afya nchini.

Hayo yamesemwa leo Septemba 21, 2024, na Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Bw. Vicent Sungusia, wakati wa kikao kazi kati ya Bohari ya Dawa (MSD) na Waganga Wafawidhi, Wauguzi Wafawidhi, pamoja na Makatibu wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Tanzania bara.

“Tumeweka mikakati madhubuti ya kuboresha mnyororo wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya. Kupitia mafunzo na uwezeshaji wa watendaji wa hospitali za rufaa na uwezo wa kusimamia rasilimali za afya.”amesema Bw.Sungusia

Aidha amesema kuwa mifumo ya ufuatiliaji wa haraka wa mahitaji ya dawa inasaidia kubaini upungufu mapema na kuchukua hatua stahiki kwani haya yote ni sehemu ya dhamira ya MSD kuhakikisha kwamba hospitali za rufaa zinatoa huduma bora kwa wagonjwa wote, bila vikwazo vya uhaba wa dawa au vifaa tiba.

Bw. Sungusia amesema, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, MSD imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kusaini mikataba ya muda mrefu na wazalishaji kwani hatua hii imepelekea ongezeko kubwa la upatikanaji wa dawa, kutoka 51% katika mwaka wa fedha uliopita hadi zaidi ya 80% mwaka huu.

“MSD inaendelea kuboresha kazi zake kwa kuimarisha utendaji wa kazi zake ili kuendelea kutoa huduma za upatikanaji wa bidhaa za dawa kwa Watanzania.” Amesema. Bw. Sungusia