Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MJADALA WA KIDIPLOMASIA YA KISAYANSI WACHUKUA NAFASI MKUTANO WA UNGA 80

Posted on: September 26th, 2025

Na WAF, New York, MAREKANI

Wizara ya Afya ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wameandaa mjadala muhimu kuhusu Diplomasia ya Kisayansi katika Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa (UNGA 80) unofanyika jijini New York, Marekani.

Mjadala huo umewakutanisha viongozi wa Serikali kutoka Afrika, watafiti, wawakilishi wa taasisi za kikanda na washirika wa maendeleo kwa lengo la kuangazia nafasi ya sayansi katika kuimarisha mifumo ya afya, kuchochea uvumbuzi, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa maendeleo endelevu ya bara la Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, Septemba 25,2025 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Afya, Bw. Ismail Rumatila, amesisitiza umuhimu wa kutumia matokeo ya tafiti za kisayansi kutengeneza suluhisho la changamoto halisi, ikiwemo kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa nje.

Bw. Rumatila amezitaja taasisi kama MUHAS na ECSA-HC kuwa mifano ya mafanikio ya ubunifu wa Kiafrika ambayo bara la Africa linapaswa kujivunia na kuyaendeleza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dkt. Ntuli Kapologwe, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uwekezaji wa uwezo wa kisayansi barani Afrika, huku akibainisha kuwa, ingawa Afrika inabeba zaidi ya asilimia 25 ya mzigo wa magonjwa duniani, bara hilo linachangia chini ya asilimia mbili (2) ya machapisho ya kisayansi na hupokea chini ya asilimia moja (1) ya ufadhili wa utafiti na maendeleo (R&D).

Dkt. Kapologwe amefafanua kuwa ECSA-HC iko mbioni kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Sayansi na Ubunifu jijini Arusha, kitakacholenga kukuza tafiti na uvumbuzi kama njia ya kudhibiti changamoto za kiafya barani Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, akihitimisha mjadala huo kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango yeye amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na jumuiya za kisayansi ni muhimu ili kuifanya sayansi kuwa dira ya maendeleo ya Afrika.