Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MILA POTOFU, ELIMU DUNI KICHOCHEO MARADHI YA KINYWA NA MENO

Posted on: May 2nd, 2024



Na WAF, GEITA

Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga Anord Joachim, amesema elimu duni na imani potofu kutoka kwa baadhi ya watu imekuwa kichocheo cha kuongezeka kwa wagonjwa wa kinywa na meno mkoani humo.

Akizungumza kwenye kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia iliyoweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita amesema, watu wengi wanafika hospitalini wakiwa wamechelewa na wakiwa katika hali mbaya.

"Wapo watu wanaofika wakiwa kwenye hatua za mwisho kabisa na pengine tayari ameshapata maambukizi na vimelea vya kansa ya kinywa hali inayosababisha kuwafanyia upasuaji kuondoa hata taya.

Dkt. Anord anasema, kutokana na habari wanazozipata mtaani bila kuwafuata wataalam ndio imekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la tatizo hilo.

"Amefika mgonjwa kwenye kambi hii akitokea eneo moja hapa Geita, anasema aliambiwa kadri uvimbe kwenye shavu unavyo ongezeka ndio kupona kumekaribia kitu ambacho sio cha kweli". Amesema Dkt. Anord.

Dkt. Anord ameiasa jamii, kuwaona wataalam waliosomea taaluma ya kinywa na meno na sio watu wengine ambao hawana utaalamu huo.

Aidha, Dkt. Anord ametumia fursa hiyo kuendelea kuwaasa wanachi kujitokeza kwa wingi na kutumia kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia ambao wapo mkoani Geita kuanzia tarehe 29 Aprili hadi 03 Mei, 2024 kwa ajili ya kupatiwa Matibabu na elimu juu ya afya zao.

Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapo mkoani Geita wakiwa na Kaulimbiu TUMEKUFIKIA, KARIBU TUKUHUDUMIE

MWISHO