Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAANZISHA HUDUMA YA USINGIZI PANGANI

Posted on: October 24th, 2024

Na WAF - Pangani, Tanga

Madaktari Bingwa wa Rais Samia waliopo katika Hospitali ya wilaya ya Pangani Jijini Tanga wawezesha kutumika na kufungwa kwa mashine ya usingizi na ganzi baada ya kutoa mafunzo kwa watumishi waliopo katika Hospitali hiyo.

Mashine hiyo imefungwa na kuanza kutoa huduma leo Oktoba 23, 2024 katika Hospitali ya Wialaya ya Pangani kupitia kambi ya siku sita ya matibabu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia waliopo Wilayani humo.

Akizungumza mara baada ya kufunga mashine hiyo ya usingizi na ganzi salama Daktari Bingwa wa usingizi na ganzi salama kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Rashid Mohammed amesema mashine imechukuliwa kutoka kituo cha afya cha jirani na haikuwa ikitumika kutokana na ukosefu wa mtaalamu wa kutumia mashine hiyo.

“Mashine ilikuwa imekaa tu na hawakuwa wakiitumia hivyo baada ya kuja katika awamu ya kwanza tuliichukua na kambi ya awamu hii tumewaelekeza namna ya kuifunga na namna ya kuitumia ili waweze kutoa huduma za usingizi salama kwa wananchi wanapokuja hospitalini hapa kufanyiwa upasuaji,” amesema Dkt. Rashi.

Akizungumza mmoja wa watumishi waliopatiwa mafunzo hayo kutoka hospitali hiyo ya Wilaya ya Pangani Bi. Tusajigwe Mdamu ambaye ni muuguzi wa usingizi na ganzi amesema baada ya mafunzo hayo na kufungwa kwa mashine hiyo kutawezesha kupunguza rufaa za upasuaji kwa wananchi.

“Kutokana na hapo awali tulikuwa tukitumia dawa za usingizi na kuna baadhi ya pasuaji tulikuwa hatufanyi lakini baada ya kupewa mafunzo ya namna gani ya kutumia mashine hii ya usingizi na ganzi tutaweza kufanya pasuaji zote hapa hapa bila kutoa rufaa ya kwenda hospitali ya Bombo Tanga au Muhimbili,” bi. Tusajigwe.

Aidha, ameongeza kwa kushukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusambaza madaktari bingwa hao ambao wanasaidia kusongeza hudum za kibingwa karibu na wananchi na kuwapunguzia adha ya kutafuta huduma za afya kwa gharama na umbali mrefu na kuongeza kuwa uwepo wa madaktari hao pia unanufaisha watumishi waliopo katika hospitaki za wilaya wanazokwenda hali inayochagiza kuboresha kwa huduma za afya kwa Watanzania.