Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI YAMEPUNGUA MKOANI TANGA HADI KUFIKIA 2.9%

Posted on: February 23rd, 2024



Na. WAF - Tanga

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na juhudi kubwa za mapambano dhidi ya ongezeko la maambukizi mapya ya VVU ambapo kwa Mkoa wa Tanga kiwango cha maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI yamepungua hadi kufikia 2.9% ukilinganisha na 4.4% ya Kitaifa.

Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo jana Februari 23, 2024 wakati akipokea na kukabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Tsh: Milioni 800 kutoka kwa wadau wa Sekta ya Afya CDC kupitia THPS kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI na Kifua Kikuu katika Mkoa wa Tanga.

“Hata kama maambukizi yamepungua katika Mkoa wetu, tusibweteke, tunaomba kila mmoja wetu apime Virusi vya UKIMWI ili aweze kujua hali ya maambukizi na ukigundulika una maambukizi tunakuanzishia dawa ili uendelee kuishi maisha mazuri.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, katika kila watu 100 wanaotumia dawa za kufubaza makali ya UKIMWI katika Mkoa wa Tanga, watu 98 wamefubaza makali ya Virusi vya UKIMWI na kupelekea kupunguza nafasi ya kumuambukiza mwengine.

Aidha, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Simeo ikiwa ni pamoja na kuweka nguvu ya kuwafikia watu wanaotumia dawa za kulevya na wanaojidunga sindano ili kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.

Agizo jingine amesema, ni kuongeza jitihada za kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka Kwa mama kwenda kwa mtoto na Ushirikishwaji wa jamii, viongozi wa dini na waganga wa jadi katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

“Tunataka hadi kufika Mwaka 2025 tufikie asilimia 95, yani katika kila watu 100 wenye Virusi vya UKIMWI angalau asilimia 95 wawe wanajua kwamba wana maambukizi ya VVU ambapo kwa Mkoa wa Tanga hadi sasa ni asilimia 82 katika kila watu 100 wanaojua hali zao.” Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy ametoa wito kwa Wanaume kutoogopa kupima virusi vya UKIMWI na kusubiri majibu ya wake zao au wenza wao na kudhani ni majibu yao, kila mtu akapate vipimo vyake na majibu yake kwa kuwa inawezekana mwenza wako ana maambukizi wewe hauna au wewe unayo mwenza wako hana.