Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI MOUNT MERU YATAKIWA KUIMARISHA ULEZI VITUO VYA AFYA

Posted on: April 15th, 2024



Na WAF, Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, ametoa wito kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, kuimarisha ulezi wa vituo vyote vinavyotoa huduma za afya ikihusisha huduma za mkoba na mafunzo kwenye utoaji wa huduma za afya ili kuimarisha na kuboresha huduma za afya.

Dkt. Jingu ameyasema hayo leo, Aprili 15, 2024 Mkoani Arusha wakati wa ziara yake katika Hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia hali ya utoaji huduma.

“Tuimarishe ulezi wa vituo vingine vyote vinavyotoa huduma za afya hapa mkoani na ulezi huku mkihusisha huduma za mkoba na mafunzo katika vituo vya kutolea huduma za afya". Amesema Dkt Jingu

Pia, Dkt. Jingu Amesema  ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, Mount Meru inatakiwa kuwa Hospitali kiongozi katika mkoa huu kwa kuwajengea uwezo watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa kulea vituo vingine chini ya uongozi wa Hospitali ya Mount Meru kutahakikisha mkoa mzima unanufaika na viwango vya juu vya huduma za afya. 

"Ulezi huu hautahusisha tu upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu bali pia mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wa afya ili kuendeleza stadi zao na kuboresha huduma wanazotoa" amesisitiza Dkt. Jingu.

Awali akisoma taarifa ya Hospitali Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru Dkt. Kipapi Mlambo amemshukuru Dkt. Jingu kwa kutembelea hospital hiyo na kukagua hali ya utoaji wa huduma kwani kufanya hivyo ni chachu ya watumishi katika sekta ya afya kufanya kazi kwa weledi zaid.