Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

FEDHA ZA MIRADI ZITUMIKE KWA MALENGO YALIYOKUSUDIWA

Posted on: October 26th, 2024

Na WAF – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wadau wa maendeleo wanaosimamia miradi ya afya nchini, kuhakikisha wanatumia fedha za miradi hiyo kwa malengo husika ili kukidhi haja ya wanufaika wa miradi nchini.

Dkt. Mollel ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Duniani, yaliyofanyika leo tarehe 25 Oktoba, 2024 katika viwanja wa Chuo kikuu cha Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam.

“Natoa msisitizo kwa wadau wote nchini kutumia fedha za miradi kwa malengo na walengwa waliokusudiwa ili kuisaidia jamii yenye uhitaji na ufadhili na mradi huo ambapo natoa pia angalizo na onyo kwa wadau wanaotumia fedha za miradi hiyo kwa maslahi yao binafsi,” amesema Dkt. Mollel.

Awali akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi Msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza Dkt. Omari Ubuguyu amesema Serikali imeendelea kuongeza vituo vya kutolea huduma za matibabu ya ugonjwa huu, kwani awali ilikuwa ni Hospitali ya Taifa ya Mifupa na Ubongo (MOI) pekee iliyokuwa ikitoa matibabu haya lakini baadae Serikali imewezesha hospitali zingine za kanda kutoa matibabu haya kama vile hospitali za Kanda za Bugando, Mbeya, KCMC, na BMH vilevile hospitali ya Hydom Manyara na Arusha Lutheran Hospital.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wazazi wa watoto wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo wazi Bw. Ramadhan Mwaluko ameitaka jamii kuacha dhana potofu dhidi ya watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi ikiwa ni pamoja na kuwafichua watoto hao ili kupata haki zao za msingi kama vile huduma za afya na masomo.