Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. JINGU AWATAKA MADAKTARI BINGWA KUKAA VITUONI

Posted on: April 30th, 2024



Moshi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka Madaktari Bingwa nchini kukaa katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa ili kuwezesha wananchi kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao.

Dkt. Jingu amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi iliyopo mkoani Kilimanjaro ikuwa ni sehemu ya ziara yake kuangalia hali ya utoaji wa huduma za afya.

Dkt. Jingu ameipongeza Hospitali hiyo kwa huduma bora inazotoa kwa wananchi huku akiwataka Madaktari bingwa kujitoa zaidi kuwasaidia wananchi na kuwataka wauguzi kuwatumia vyema madaktari hao katika kushauriana namna ya kuwahudumia wananchi ili kufikia azma ya utoaji bora wa huduma za afya.

“Ni vizuri wataalam wa afya mkashauriana namna masuala mbalimbali ya taaluma na kupeana uzoefu, Serikali imewekeza kwenye miundombinu, watumishi, vifaa na vifaa tiba lengo likiwa ni kutoa huduma za afya kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo hivyo kupitia nyie wataalam huduma zitaendelea kuimarika”. Amesema Dkt. Jingu.

Aidha, Dkt. Jingu amesema kuwa wananchi hivi sasa wanahitaji huduma za kibingwa hapa nchini ili waweze kuokoa gharama za kufuata huduma hizo nje ya nchi, hivyo ili huduma hizo ziweze kupatikana kwa ufanisi zinahitaji uwepo wa wataalam wakiwemo Madaktari na bobezi.

Hata hivyo Dkt. Jingu amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa mawenzi ina jukumu wa kuzilea Hospitali zilizo chini yake huku akionesha kufurahishwa na dawati la huduma kwa wateja na kusisitiza kuwa lugha nzuri ndiyo muhimili mkuu wa mawasiliano kwa wananchi huku akiongeza Serikali ina matumaini makubwa na watumishi na pia wajitahidi kuongeza ubunifu kwa kila wanachokifanya na kuangalia huduma za kuongeza ili Hospitali iwe bora zaidi.