BMH YATAKIWA KUTEGUA KITENDAWILI ILI IWE HOSPITALI YA TAIFA
Posted on: August 9th, 2024
Na WAF - DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameitaka Hospitali ya Kanda ya Kati ya Benjamini Mkapa kuendelea kuboresha zaidi hali ya utoaji na ubora wa huduma hususani zile za kibingwa na ubingwa bobezi ili iweze kupanda hadhi na kuwa Hospitali ya Taifa.
Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo Agosti 9, 2024 wakati wa Ziara yake iliyolenga kutembelea Hospitali ya Benjamini Mkapa na kujionea utoaji wa huduma kwenye hospitali hiyo, ambapo akiwa hospitalini hapo amewasisitiza wataalamu hao kuona namna gani wanaboresha huduma ili kufikia hadhi ya Taifa.
“Hospitali ya Taifa kama mnavyofahamu kazi yake kubwa ni Kutoa huduma Bobezi na Ubora wa Huduma, sasa hapa tayari Mnahuduma za kutosha, Lazima tupambane usiku na mchana ili hospitali hii ipande hadhi na kuwa hospitali ya Taifa, amesema Dkt. Jingu na kuongeza
"BMH ni hospitali kubwa katika makao makuu ya nchi, katika hospital ya taifa ili iweze kutoa huduma zinazotakiwa kwa mazingira haya ya Makao Makuu ya Nchi, sasa lazima tuwe kituo ambacho kitaweza kukidhi mahitaji ya kitaifa zaidi na kutoa huduma hizo” amesisit8za Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu Amesema njia pekee itakayo iwezesha Hospitali hiyo kupata hadhi ya Taifa ni wataalamu wa Hospitali kuziimarisha zaidi huduma mbalimbali inazotoa hususani zile za kibingwa na ubingwa bobezi.
“Lazima tuone namna gani tunaboresha zaidi huduma zetu katika Hospitali ya Benjamini Mkapa na naona tayari mmeshaonyesha jitihada, hapa kuna huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, tayari mna huduma kama 20 ukiacha zile nane ambazo ni Bobezi ” amesema Dkt. Jingu.
“Kwa kuzingatia kuwa sisi ni watu wa familia moja, Kuna faida za Mashirikiano nazo ni nyingi ikiwemo wanafunzi wanaotoka Chuo kikuu cha Dodoma watapata sehemu sahihi za kujifunzia na bahati nzuri tatari mnawapa nafasi, na mwisho wa siku kama nchi tutanufaika maamuzi na tutapata watu ambao wameiva” Amesema Dkt. Jingu.
Akiwa hapo Dkt. Jingu pia ametembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha Kansa Mradi wenye thamani ya Shilingi Bilioni 28 ambapo pia amemtaka Mhandisi wa mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati bila kuthiri ubora wa Mradi huo.