Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ALIYE KAA BILA KUSIKIA KWA MIAKA MINNE, HATIMAYE MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAMTIBU.

Posted on: May 2nd, 2024



Na WAF, GEITA

Masanja Maduhu mkaazi Bariadi mkoani Simiyu aliyekaa bila kusikia kwa miaka Minne, amefanikiwa kusikia mara baada yakupatiwa tiba na Madaktari Bingwa na Bobezi walioweka kambi mkoani Geita.

"Nilianza kwenda kwa mganga wa kienyeji ambaye alisema kuna watu wamenichezea nikalipa elfu 50 ili anitibu lakini sikufanikiwa kupona" amesema Maduhu.

Maduhu ambaye ni mkulima na Mfugaji wa Bariadi, amesema tatizo lake lilianza miaka minne iliyopita, lakini hakuweza kwenda hospitalini akiamini huenda mara baada yakutumia dawa ya Mganga wa kienyeji angeweza kupona.

Akizungumza mara baada yakumpatia tiba Daktari Bingwa wa Masikio, pua na koo Richard Shija wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera,.amesema mgonjwa huyo alifika hospitalini hapo akiwa shida yakutosikia na baada ya uchunguzi kwakutumia kifaa kiitwacho ENT endoscopy walibaini sikio lake kuwa na nta ikiyozidi kiwango na usaha.

"Mbali na kuziba sikio tayari lilikuwa limetengeneza maambukizi (infections) ilizalisha usaha ambapo kama asingechukua hatua za haraka ndani wiki kadhaa zijazo tatizo lingekuwa kubwa na ingebidi afanyiwe upasuaji" amesema Dkt. Shija.

Katika siku nne za Madaktari Bingwa wa Samia kwa Kanda hiyo ya ziwa, Idara hiyo inayojihusisha na masikio, pua na koo imefanikiwa kuwahudumia wananchi wasio pungua 80.

Mara baada yakupatiwa matibabu hayo, Mabula ametumia fursa hiyo, kuiasa jamii kuepukana na mila potofu na badala yake wakipata changamoto wafike kwa wataalam wa afya.

Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan ipo Kanda ya ziwa mkoani Geita kuanzia tarehe 29 Aprili, hadi tarehe 03 Mei, 2024 wakitembea na Kauli mbiu Tumekufukia, Karibu Tukuhudumie

Mwisho