Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAJENGA UWEZO WA WATUMISHI WA AFYA MISENYI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO

Posted on: September 25th, 2026

Na Happyness Hans, WAF-Kagera

Watumishi wa afya katika Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera wamejengewa uwezo na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya katika kukabiliana na wagonjwa wa dharura na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola. Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa, ujuzi na utayari wa watumishi katika kutoa huduma salama na bora kwa wananchi pindi magonjwa ya milipuko yanapotokea.

Amesema hayo leo 25, 2026 mkoani kagera, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, Dkt. Daniel Chochole, amesema wamefarijika kupata timu hiyo ya wataalamu kutokana na umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi wa afya, hasa kwa kuzingatia jiografia ya wilaya hiyo ambayo ipo karibu na nchi jirani zilizowahi kukumbwa na magonjwa ya milipuko. Amesema mafunzo hayo yatawasaidia watumishi kuwa tayari kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Dkt. Chochole ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kupeleka timu hiyo wilayani Misenyi, huku akiomba Serikali kuongeza idadi ya watumishi wa afya katika wilaya hiyo kutokana na kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watumishi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kabyaile, Dkt. Samson Joseph, amesema mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwa watumishi, hususan wale wapya walioajiriwa, kwa kuwa yamewajengea uwezo na kuwaongezea ujasiri wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Amesema watumishi wamekumbushwa umuhimu wa kufuata miongozo ya Kinga na Udhibiti wa Maambukizi (IPC) ili kujikinga wao wenyewe na kuzuia maambukizi kwa wengine, amesema kwa sasa kituo hicho kiko tayari kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo yatatokea.

Naye Muuguzi wa Kituo cha Afya Kabyaile, Bi. Happyness Tibaijuka, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa watumishi kwa kuwa wamepata fursa ya kujifunza mambo mapya, kukumbushwa yale waliyokuwa wameyasahau na kupata maelekezo yatakayowawezesha kuwa na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko na kujilinda endapo ugonjwa utatokea.