Wizara Ya Afya

TANZANIA YAMUENZI DKT. SENAIT FISSEHA KWA MCHANGO WAKE KATIKA AFYA YA WANAWAKE

Posted on: September 26th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Addis Ababa

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali ya Tanzania inathamini mchango mkubwa wa Dkt. Senait Fisseha katika kuimarisha afya ya wanawake, afya ya uzazi na mifumo ya afya barani Afrika pamoja na wadau wengine katika sekta ya afya.

Dkt. Samizi amesema hayo leo Agosti 26, 2026 katika hafla ya kumuenzi Dkt. Senait Fisseha iliyofanyika katika Makao Makuu ya Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), jijini Addis Ababa, Ethiopia.

"Uongozi, maono na kujitolea kwa Dkt. Senait vimekuwa na mchango wa kudumu katika afya duniani, hususan katika kuendeleza afya na haki za uzazi na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika," amesema Dkt. Samizi

Aidha, Dkt. Samizi ametoa pongezi kwa Susan Thompson Buffett Foundation kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha sekta ya afya ambapo tangu mwaka 2022, Tanzania imepokea jumla ya Dola za Marekani milioni 51.8, huku makubaliano ya ziada ya Dola milioni 15 yakisaini na kufikisha jumla ya ahadi ya ufadhili wa Dola milioni 66.8.

Ameeleza kuwa msaada huo umechangia kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, vijana pamoja na kuboresha miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Pia, Dkt. Samizi amesema uwekezaji huo umewezesha kuwajengea uwezo watumishi wa afya wapatao 13,000 na kuwafikia takribani wahudumu wa afya wa jamii 4,500.

Vilevile, amesema ushirikiano huo umechangia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo watu 8,000 wamenufaika, pamoja na kusambaza mifumo ya Kielektroniki ya Taarifa za Wagonjwa (Electronic Medical Records) katika vituo vya afya 167.