TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHA HUDUMA ZA CHANJO, KUWAFIKIA WATOTO WOTE
Posted on: September 25th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Addis Ababa
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe, wameshiriki kikao cha pembezoni mwa Mkutano wa 76 wa WHO-AFRO, kilichoandaliwa na GAVI jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza kiwango cha uchanjaji na kuhakikisha watoto wote nchini wanapata huduma za chanjo.
Katika kikao hicho Dkt. Samizi ameshiriki kama mtoa mada (panelist) na kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika huduma za chanjo ambapo kwa Mwaka 2024 kiwango cha chanjo ya DTP-HepB-Hib dozi ya tatu kilifikia asilimia 96, MR1 asilimia 99.8 na MR2 asilimia 94, chanjo dhidi ya HPV uliwafikia wasichana milioni 5.48 wenye umri wa miaka 9–14.
Katika kikao hicho, Dkt. Samizi amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha huduma za chanjo na kuongeza kiwango cha uchanjaji hususan kwa watoto wanaoishi maeneo ya vijijini, maeneo ya pembezoni na jamii ambazo ni vigumu kufikiwa.
Aidha, Dkt. Samizi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuongeza mchango wa ndani katika kugharamia huduma za chanjo, huku ikiimarisha mifumo ya utoaji huduma, ufuatiliaji na matumizi ya takwimu ili kuwafikia watoto ambao bado hawajapata chanjo au hawajakamilisha chanjo zao.
Pia, Dkt. Samizi ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Gavi kwa ushirikiano na msaada wake unaoendelea kwa Tanzania, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia katika kuimarisha huduma za chanjo na afya ya umma nchini.
Amesema, Tanzania inalenga kuhakikisha kuwa kiwango cha uchanjaji kinaendelea kuwa cha juu na chenye usawa katika jamii zote ili kila mtoto anayehitaji chanjo aweze kuipata bila kujali anaishi eneo gani.