Wizara Ya Afya

TANZANIA, GATES FOUNDATION KUSHIRIKIANA KUIMARISHA MFUMO WA SEKTA YA AFYA NCHINI

Posted on: September 26th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Addis Ababa

Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan inathamini ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali na Taasisi ya Kimataifa ya Gates Foundation katika kuimarisha huduma za afya, hususan afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Agosti 26, 2026 katika kikao cha pande mbili kati ya Tanzania na Mkurugenzi wa Taasisi ya Gates Foundation Ukanda wa Afrika Dkt. Paulin Basinga, kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO-AFRO), jijini Addis Ababa, Ethiopia.

"Tanzania inatambua mchango wa Gates Foundation katika kuimarisha programu za afya nchini ikiwemo afya ya mama na mtoto mchanga, malaria, lishe na uzazi wa mpango, huku ushirikiano huo ukichangia kuboresha viashiria vya afya nchini," amesema Dkt. Magembe

Amesema, Tanzania inathamini pia miradi inayoendelea kwa ushirikiano na Gates Foundation ikiwemo 'THAMINI UHAI' katika afya ya mama na mtoto mchanga, afua za lishe, Knowledge Translation Hub, matumizi ya Ultrasound yenye teknolojia ya AI, NEST360 pamoja na Beginnings Fund.

Aidha, Dkt. Magembe ameomba Gates Foundation kuendelea kuongeza ushirikiano katika utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika unaolenga kufikia malengo matatu ya sifuri ikiwemo kutokuwepo kwa kujifungulia nyumbani, kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto mchanga vinavyoweza kuzuilika, na kutokuwepo kwa mtoto asiyechanjwa.

Katika eneo la lishe, Dkt. Magembe ameomba Gates Foundation kusaidia uanzishwaji wa vituo vya Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) katika vituo vya afya na jamii, kuimarisha programu za uongezaji virutubishi kwenye chakula na kuongeza uhamasishaji wa jamii kuhusu lishe ya watoto.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa virutubishi vya aina mbalimbali (MMS) na kuhakikisha manunuzi yake yanaendana na taratibu za Bohari ya Dawa (MSD), ili kuimarisha huduma za lishe na afya ya mama na mtoto nchini.