BONANZA LA JIONGEZE360 LATOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA TUNDURU
Posted on: September 26th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Tunduru
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, kupitia Programu ya Afya ya Uzazi kwa Vijana, imeendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana balehe kupitia Bonanza la Jiongeze360, lenye lengo la kuwapatia vijana taarifa na elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Bonanza hilo linafanyika katika Mkoa wa Ruvuma, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, kuanzia leo Agosti 26, 2026, na linatarajiwa kutamatika Agosti 28, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Dkt. Wilfred Rwechungura, ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Afya kwa kupeleka bonanza hilo Wilayani humo, akieleza kuwa litasaidia kuwafikia vijana wengi na kuwapatia elimu ya afya ya uzazi ili wawe na uelewa mpana kuhusu masuala yanayohusu afya zao.
Dkt. Rwechungura amesema Tunduru ni miongoni mwa Wilaya zinazokabiliwa na changamoto ya mimba za utotoni, hali inayosababisha baadhi ya watoto kuacha shule, pamoja na changamoto ya ukatili wa kijinsia.
Ameeleza kuwa kufanyika kwa bonanza hilo Wilayani humo kutasaidia kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa vijana, hatua itakayochangia kupunguza changamoto hizo.
“Nimetaarifiwa kuwa bonanza hili litafanyika kwa siku tatu na litaambatana na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi, lishe na afya ya akili, pamoja na utoaji wa huduma za afya kama vile upimaji wa VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na huduma za uzazi wa mpango. Hivyo, vijana watapata fursa ya kujengewa uelewa mpana kuhusu masuala mbalimbali ya kiafya yanayowakabili,” amesema Dkt. Rwechungura.
Ameongeza kuwa bonanza hilo ni jukwaa muhimu kwa vijana kujifunza, kuuliza maswali na kujua hali ya afya zao, jambo litakalowasaidia kufanya maamuzi sahihi, kujilinda dhidi ya changamoto mbalimbali za kiafya na kujua mahali pa kupata msaada wanapokutana na changamoto.
Dkt. Rwechungura ametoa rai kwa vijana wa Wilaya ya Tunduru kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kushiriki katika shughuli za bonanza na kupata elimu ya kina kuhusu masuala mbalimbali ya afya, hususani afya ya uzazi, pamoja na kutumia huduma za upimaji wa afya zinazotolewa