KILA DAKIKA NI MUHIMU KATIKA KUOKOA MAISHA - WAZIRI MCHENGERWA
Posted on: August 24th, 2026NA Cletus Sanga, WAF - Kibaha
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema kila dakika katika huduma za dharura ina thamani na inaweza kuwa tofauti kati ya uhai na kifo au kati ya kupona na kupata ulemavu wa kudumu.
Akizungumza leo Agosti 24, 2026 wakati wa makabidhiano ya gari la wagonjwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Mchengerwa amesema ambulance hiyo itasaidia kuwafikia na kuwasafirisha kwa usalama wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Amesema huduma hiyo ni muhimu kwa wajawazito wenye dharura, watoto wachanga, waathirika wa ajali, wagonjwa wenye matatizo makali ya kupumua, magonjwa ya moyo, kiharusi na dharura nyingine mbalimbali.
Mhe. Mchengerwa amesema kwa wananchi wa Kibaha na maeneo jirani, uwepo wa ambulance hiyo utasaidia kupunguza ucheleweshaji wa rufaa, kuongeza usalama wa wagonjwa wakati wa safari na kurahisisha uunganishaji wa kituo hicho na hospitali zenye huduma za juu zaidi.
Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha gari hilo linafanyiwa matengenezo kwa wakati na kutengewa bajeti ya mafuta, matengenezo, matairi, betri, bima na mahitaji mengine muhimu ili liwe tayari muda wote.
Amesema, mafanikio ya huduma za dharura hayatapimwa kwa idadi ya magari yaliyokabidhiwa pekee, bali kwa idadi ya magari yaliyo tayari kufanya kazi, wagonjwa waliofikiwa kwa wakati na maisha yaliyookolewa.