SERIKALI YAWEKA MKAKATI MPYA WA KUSIMAMIA NA KUENDELEZA VIFAA TIBA
Posted on: August 27th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua Mwongozo wa Mipango ya Sekta ya Afya kuhusu matengenezo, uingizwaji na uondoaji wa vifaa tiba pamoja na kujenga uwezo wa Wahandisi, Mafundi wa Vifaa Tiba na watumiaji wa vifaa hivyo, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa vifaa tiba na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo huo leo Agosti 27, 2026 Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakim, amesema Serikali imewekeza takribani Shilingi trilioni 1.2 katika vifaa tiba kwenye vituo vya afya vya umma 7,688 hadi Oktoba 2025, akieleza kuwa mwongozo huo umeandaliwa kutokana na umuhimu wa kuhakikisha vifaa hivyo vinaendelea kufanya kazi kwa ufanisi.
Dkt. Eliakim amesema mwongozo umeweka mfumo wa kusimamia mzunguko mzima wa maisha ya vifaa tiba, kuanzia matengenezo, uingizwaji, uondoaji hadi kujenga uwezo wa wataalamu na watumiaji, ili kupunguza muda ambao vifaa vinakuwa havifanyi kazi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya.
“Tunapaswa kubadilisha utaratibu wa kusubiri kifaa kiharibike ndipo kifanyiwe matengenezo. Tunahitaji kuimarisha matengenezo kinga, kupanga uingizwaji wa vifaa kwa wakati na kuhakikisha vifaa vilivyofikia mwisho wa matumizi vinaondolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema Dkt. Eliakim.
Aidha, Dkt. Eliakim amesema mwongozo unaelekeza kila kituo cha kutolea huduma za afya kuwa na mpango na bajeti ya matengenezo ya vifaa tiba, pamoja na mpango wa uingizwaji na uondoaji wa vifaa, huku msisitizo ukiwekwa katika kujenga uwezo wa Wahandisi, Mafundi wa Vifaa Tiba na watumiaji wa vifaa hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Matengenezo ya Vifaa Tiba, Dkt. Alex Magesa, amesema utekelezaji wa mwongozo huo utasaidia kuimarisha mfumo wa matengenezo ya vifaa tiba nchini na kuongeza muda wa matumizi ya vifaa vilivyopo katika vituo vya kutolea huduma za afya.