TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHA KINGA, MAANDALIZI NA MWITIKIO WA DHARURA ZA AFYA
Posted on: August 27th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa
Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha afua za kinga ikiwemo kujiandaa na kukabiliana na dharura za afya leo Agosti 27, 2026 katika Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani, unaoendelea jijini Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa mawasilisho kutoka kwa Wakurugenzi Wizara ya Afya, ikiwa ni sehemu ya ujumbe ulioyongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi
Tanzania imewasilisha hatua zilizofikiwa katika kuimarisha Timu ya Taifa ya Dharura za Afya (National EMT), ikiwemo kuwa na wataalamu 44 waliopatiwa mafunzo na kuwepo mpango wa kutoa mafunzo kwa wataalamu 350 zaidi katika kanda saba ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza uwezo wa mwitikio wa haraka wakati wa dharura za kiafya.
Katika mawasilisho hayo, Tanzania imeunga mkono Mkakati wa Kikanda wa Timu za Dharura za Afya (EMTs) 2026–2030 na Mkakati wa Utekelezaji wa Maboresho ya Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR-2005) wa mwaka 2026-2030 huku ikisisitiza kuimarisha uwezo wa nchi kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa, majanga na dharura nyingine za kiafya.
Katika eneo la chanjo, Tanzania imewasilisha hatua zinazoendelea kuchukuliwa na kuwezesha kuenea kwa chanjo kuwa zaidi ya asilimia 90 kwamuda wote ambapo kwa sasa, Tanzania inakamilisha mpango mkakati wa huduma za chanjo unaokwenda sambamba na Agenda ya Chanjo ya Kimataifa yam waka 2026 hadi 2030 (Immunization Agenda 2030).
Pia, wasilisho hilo limeeleza taarifa ya hivi karibuni ya viashiria vya afya ya uzazi na mtoto, imeonesha kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia 40%, ambapo ni matokeo ya kupungua kwa magonjwa yanayokingwa na chanjo, Hivyo Jamii inasisitizwa kuhakisha kila mtoto anaestahili kupata chanjo anapelekwa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kupata chanjo.
Aidha, Tanzania imependekeza kuimarishwa kwa uratibu na ushirikiano wa kikanda ili kuwezesha nchi za Afrika kuwa na msimamo wa pamoja na mifumo madhubuti ya kukabiliana na changamoto na dharura za afya zinazovuka mipaka ya nchi.