Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU WAJADILI MFUMO WA KUONGEZA UFANISI UPATIKANAJI WA RASILIMALI WATU NA FEDHA SEKTA YA AFYA

Posted on: September 27th, 2026

Na Mvuda Jaffer;WAF-Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na shirika lisilo la kiserikali la ICAP wameanza kujadili uanzishwaji wa Mfumo wa Tanzania Resource and Talent Hub unaotarajiwa kusaidia kutambua na kuunganisha mahitaji ya rasilimali fedha na watu katika Sekta ya Afya na fursa za rasilimali fedha zinazotangazwa kutoka katika taasisi mbalimbali duniani,kwa lengo la kuongeza uwezo wa Serikali na wadau wa Sekta ya Afya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati na vipaumbele vya afya nchini.

Daktari Mkuu na Mratibu wa Afya ya Msingi kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Sungwa Kabissi, amesema hayo leo Agosti 27, 2026 wakati wa kikao cha kutoa maoni kuhusu Mfumo wa Tanzania Resource and Talent Hub kilichofanyika Mkoani Mwanza.

“Kwa ujumla, Tanzania Resource and Talent Hub itakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa utafutaji na matumizi ya rasilimali fedha kuimarisha ushirikiano na wadau na kuongeza kasi ya utekelezaji wa vipaumbele vya Sekta ya Afya hivyo kuchangia ujenzi wa mfumo wa afya wenye uwezo endelevu na unaokidhi mahitaji ya wananchi ikiwa itafanikiwa kuundwa na kuendeshwa kwa kuzingatia vigezo vya ujengaji na uendeshaji wa serikali.” amesema Dkt. Sungwa

Naye, Mshauri wa Ufundi Masuala ya Upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU) na Kinga kutoka ICAP Tanzania Dkt. Raymond Bandio amesema msukumo wa kuanzishwa kwa mfumo huo umetokana na changamoto ya ufadhili wa kimataifa katika nyanja ya fedha hivyo, kuna haja ya kutumia fursa na miradi mbalimbali inayopatikana nchini ili kuongeza uwezo wa Serikali katika kutekeleza afua mbalimbali za afya.

“Mfumo huo unatarajiwa kuwa muhimu katika kuongeza rasilimali fedha zitakazotumika kuboresha na kutekeleza afua mbalimbali za afya nchini.” amesema Dkt. Bandio

Dkt. Bandio ameongeza kuwa kupitia mfumo huo miradi na fursa mbalimbali zinazotekelezwa nchini zitaweza kusaidia katika kuzalisha rasilimali zitakazowezesha utekelezaji endelevu wa afua za afya.