MHE. MCHENGERWA ASISITIZA USHIRIKIANO NA TAASISI ZA DINI, ARIDHISHWA NA MIRADI YA MAENDELEO ROMBO
Posted on: July 24th, 2026Na John Mapepele, WAF- Kilimanjaro
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini katika utoaji wa huduma za afya, akieleza kuwa huo ni msingi ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na unaoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo katika Hospitali ya Huruma wilayani Rombo wakati wa uzinduzi wa jengo la huduma ya dharura, Mchengerwa alisema ameridhishwa na maandalizi makubwa ya kuifanya iwe hospitali ya rufaa ya mkoa aliyoyashuhudia hospitalini hapo, akieleza kuwa yanaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Waziri huyo alisema kabla ya ziara hiyo, tayari Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimpa maelekezo mahsusi ya kuhakikisha Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Alieleza kuwa serikali zote tangu Uhuru zimeendelea kulinda na kuendeleza msingi huo, huku akibainisha kuwa suala la kushirikiana na taasisi za dini si la mtu mmoja bali ni sera ya taifa inayolenga kuwafikishia wananchi huduma bora.
Mchengerwa alisema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ili kupunguza umbali wanaolazimika kusafiri kutafuta matibabu.
Alisema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma kwa urahisi karibu na eneo analoishi.
Akizungumzia maombi yaliyowasilishwa na viongozi wa hospitali ya Huruma, Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa Rombo imepewa kipaumbele katika upatikanaji wa gari la wagonjwa (ambulance), akisema uamuzi huo umetokana na mshikamano na juhudi alizozishuhudia kutoka kwa viongozi na wananchi wa eneo hilo.