Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA KUANZISHA MFUMO WA TAIFA WA URATIBU NA MATUMIZI YA AMBULANCE

Posted on: October 4th, 2023


Na. WAF - Dar es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha mfumo wa Taifa wa uratibu na matumizi ya magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za dharura kwa haraka. 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Octoba 4, 2023 wakati wa hafla ya kupokea magari 10 ya kubebea wagonjwa yenye thamani ya Shilingi Bil. 1.1 kutoka Serikali ya India.


“Tuna changamoto kubwa sana kwa magari ya wagonjwa kuchelewa kufika kwa wakati, kwa hiyo tunakwenda na mfumo mmoja ambao utaingiza Ambulance zote nchini”. Amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy amesema magari ya kubebea wagonjwa yataingizwa kwenye mfumo wa Bima ya Afya hivyo watu waendelee kujiunga na mifuko mbalimbali ya Bima ya Afya ili kila Mtanzania aweze kupata huduma za dharura za magari ya wagonjwa. 


Wakati akipokea magari hayo Waziri Ummy amesisitiza magari yote ya Serikali ya kubebea wagonjwa (Ambulance) lazima yawe yamekatiwa Bima ili kulinda magari hayo na yaendelee kufanya kazi.  


“Yeyeto ambae tutampa Sasa hivi gari ya kubebea wagonjwa ya Serikali, tunamwambia kalipie Bima kwanza ili kulinda magari haya na yaendelee kufanya kazi”. Amesema Waziri Ummy


Vilevile Waziri Ummy amewataka madereva wa magari yote ya kubebea wagonjwa kuzingatia sheria, taratibu na matumizi sahihi ya kuendesha magari hayo ikiwemo kupakia wagonjwa tu na sio vinginevyo. 


“Tumepata taarifa kwa baadhi ya magari ya kubebea wagonjwa yanabeba vitu ambavyo ni kinyume na taratibu za magari hayo, magari haya ni ya kubebea wagonjwa tu hayapaswi kubebea vitu vingine”. Amesema Waziri Ummy