WEKENI MIKAKATI YA PAMOJA KWA WATANZANIA KUTUMIA MAJI SAFI NA SALAMA
Posted on: July 16th, 2025
Na WAF, Morogoro
Wataalam wa Afya Mazingira wa Halmashauri wamehimizwa kuweka mikakati ya pamoja ili kuhakikisha kila mtanzania ana uelewa sahihi juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya maji safi na salama kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Rai hiyo imetolewa Julai 16, 2025 mkoani Morogoro na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Ufuatiliaji Ubora wa Maji ya Kunywa Ngazi ya Kaya kwa Wataalam wa Afya Mazingira kutoka Halmashauri mbalimbali nchini.
Dkt. Mmbaga amesema ni muhimu kwa kila mmoja kuweka mikakati ya Kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko hasa kwa kuweka njia bora za kujikinga na kutoa taarifa.
“Tunapoweka dawa ya Klorini ni kinga inayozuia magonjwa mengine , hivyo ni muhimu kuhakikisha jamii inatambua umuhimu wa maji safi na salama na kuhakikisha inakuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara kwenye mikusanyiko ya watu na ikitokea kuna viashiria ni bora turipoti kwenye wizara na mamlaka tunazoshirikiana nazo” - amesema,” amesema Dkt. Mmbaga.
Aidha, Dkt. Mmbaga amesema takwimu zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji safi ya kunywa pamoja na hali ya vyoo bora unapofikia au unapozidi asilimia 75 uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ni nadra kutokea.
Amesema kutokana na Umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama ya kunywa, Wizara ya Afya imeona umuhimu kuandaa na kuendesha mafunzo ya upimaji na ufuatiliaji wa usalama wa maji ya kunywa .
"Hatua hii inalenga kujengea uwezo mikoa na halmashauri katika kubaini viashiria vya uchafuzi wa maji na kuchukua hatua stahiki kabla ya kutokea kwa mlipuko na hii ndio dhana ya Kinga ni Bora kuliko Tiba na hivyo tunataka kuona hatua za kuzuia milipuko zinachukuliwa mapema na kwa kiwango cha kutosheleza kwani upatikanaji wa maji safi ya kunywa pamoja na hali ya vyoo bora unapofikia 75% ni nadra kutokea kwa Kipindupindu,” - amefafanua Dkt. Mmbaga.
Kwa upande wake ,Mkuu wa Sehemu ya Chakula Salama, Maji Salama na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Bw. Anyitike Mwakitalima amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kila mtaalam wa halmashauri anakuwa na uelewa wa namna ya upimaji wa maji ya kunywa katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ambaye ni Mtaalamu wa Afya Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Bw. Said Ame amesema kupitia mafunzo hayo yatarahisisha kuchukua hatua za mapema katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko.