Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MIONGOZO YA RUFAA, VIWANGO VYA MSINGI MUHIMU KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: October 24th, 2025

Na WAF - Morogoro

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Mwongozo wa Rufaa za Wagonjwa na wa Viwango vya Msingi wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ni nyenzo muhimu katika kuboresha ubora na ufanisi wa huduma za afya nchini.

Dkt. Magembe amesema hayo Oktoba 22, 2025 wakati akifunga kikao kazi cha wadau wa sekta ya afya chenye lengo la kukusanya maoni kuhusu rasimu ya miongozo hiyo kilichofanyika mkoani Morogogo.

"Miongozo hii ni nyenzo muhimu katika kuboresha ubora na ufanisi wa huduma zetu za afya nchini, na marekebisho haya yanalenga kuendana na mabadiliko pamoja na mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya afya, lengo kubwa ni kuendelea kuboresha zetu," amesema Dkt. Magembe

Amesema, Miongozo inayotumika ni ya zamani hivyo ni muhimu kufanya mapitio ili iendane na hali halisi ya sasa, ikiwemo maendeleo ya miundombinu, ongezeko la watumishi na uwekezaji katika vifaa tiba.

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa Mwongozo wa Viwango vya Msingi unaainisha vigezo vya usajili, utoaji wa leseni, idadi na aina ya watumishi, pamoja na ubora wa huduma unaopaswa kufikiwa na kila kituo cha afya, huku Mwongozo wa Rufaa ukiwa ni chombo muhimu kinachoratibu mtiririko wa wagonjwa kati ya ngazi mbalimbali za huduma.

"Lakini ndugu zangu tuelewe kuwa utekelezaji wa miongozo hii inakwenda sambamba na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act), ambayo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kikwazo cha kifedha," amesisitiza Dkt. Magembe.

Pia, Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wa sekta ya afya kutoka Serikali, taasisi binafsi na mashirika yasiyo ya Kiserikali kutumia kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Afya, kutoa maoni ya kitaalam yatakayosaidia Wizara ya Afya kukamilisha miongozo hiyo kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa, Dhamira ya Serikali ni kundelea kuboresha sekta ya afya kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu, huku sekta binafsi ikiendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo hayo ambayo inaifanya Wizara ya Afya kuendelea kushirikiana na wadau.